25 Novemba 2020 - 20:03
Jordan yaitaka jamii ya kimataifa iishinikize Israel ili isitishe ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jordan amelaani vikali hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuafikii ujenzi wa nyumba mpya 540 katika eneo la Quds Mashariki unalolikalia kwa mabavu na kuitaka jamii ya kimataifa iushinikize utawala huo ghasibu ili usitishe ujenzi wake wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Dheifullah al-Fayez amesisitiza kuwa, ujenzi wa vitongoji hivyo katika maeneo ya Wapalestina unakiuka wazi sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa likiwemo azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama.

Amesema kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kuushinikiza utawala huo ghasibu ili usitishe ujenzi huo haramu wa vitongozi vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel.

Wiki iliyopita pia, Nickolay Mladenov Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Asia Magharibi aliushutumu utawala wa Kizayuni wa Israel kwa uamuzi wake wa kupanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina ya Quds Mashariki.

Aidha Kabla ya hapo Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya naye alikuwa ametoa taarifa akipinga vikali ujenzi wa vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zilizokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Huko nyuma pia Umoja wa Ulaya umewahi kueleza upinzani wake dhidi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina na hata kuutaka utawala ghasibu wa Israel usitishe ujenzi huo.

Hata hivyo uungaji mkono wa Marekani kwa Israel umekuwa ukiupa kiburi uatwala huo ghasibu na kuupandisha kichwa cha kuendelea na siasa zake za kidhalimu dhidi ya Wapalestina bila ya kujali hasira za walimwengu.

342/